UONGOZI WA JUMUIYA
ANTHONY KIMBURU - MWENYEKITI
JANE LIGOMBA - MAKAMU MWENYEKITI
ROBERT B. MUJUNI - KATIBU MKUU
ANJELINA KAVISHE - KATIBU MKUU MSAIDIZI
JOHN LIGOMBA - MHAZINI
UWAKA
ERASTO KAVISHE - MWENYEKITI
LOLINDINA - KATIBU
BAYNITT C. KILINDO - KATIBU MSAIDIZI
DANIEL NJAULE - MHAZINI
WAWATA
EDNA G. KIOGWE - MWENYEKITI
EDNA KATO - MAKAMU MWENYEKITI
MARCELINA SIMUOGOPE - KATIBU
IRENE KIMBURU - KATIBU MSAIDIZI
MAMA GONDWE - MHAZINI
VIWAWA
JIMMY GONDWE - MWENYEKITI
DAVID ANTHONY - MAKAMU MWENYEKITI
JOSEPHINE LIGOMBA - KATIBU
NEEMA KAVISHE - KATIBU MSAIDIZI
OSCAR NJAULE - MHAZINI
Ni Muungano wa Familia za Kikristo za Kikatoliki kwa Ujirani wao Kuanzia Familia Mbili hadi Kumi na Mbili zinazokutana pamoja angalau mara moja kwa wiki kwa muda wa saa moja kushirikiana katika kusali, kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari pamoja kujadili na kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kulingana na mazingira yao kwa madhumuni ya kumtafakari MUNGU na kuuishi ukristo wao kivitendo ili kuwa watakatifu.
Wednesday, 20 April 2016
Tuesday, 19 April 2016
Huduma kwa wazee na wagonjwa
Huduma kwa wazee na wagonjwa (Weekend Ministry)
Huduma kwa wazee na wagonjwa inatolewa kila Jumamosi saa 4 asbh hadi saa 11 jioni katika
viwanja vya parokia ya Segerea. Ni wajibu wetu kuwalea na kuwatunza wazee wetu kadiri neno
la Mungu linavyotuagiza. “…………….Katika neno na katika tendo, umheshimu baba yako, ili
baraka zote zikujie kutoka kwake. Mradi Baraka ya Baba itaziimarisha nyumba zao watoto, bali
laana ya mama huing’oa misingi. ……….. Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake, wala
usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa
upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; kwa maana sadaka apewayo baba
haitasahauliwa, na badala ya dhambi, itahesabiwa kwa kukuthibitisha”. (YBS 3:1-14)
Pia kwa habari ya wagonjwa na wenye shida mbalimbali, neno la Mungu linatuhimiza kuwa, “Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha
mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka
mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya” (Mk. 16:17-18). Wazee wote, wagonjwa na
wenye shida na mahitaji mbalimbali wataombewa. Waamini wote mnakaribishwa
Bernardino wa Siena
Bernardino wa Siena (8 Septemba, 1380 - 20 Mei, 1444) alikuwa mtawa wa shirika la Ndugu Wadogo na kasisi wa Kanisa Katoliki.
Alizaliwa na kubatizwa Massa Marittima (Siena) tarehe 8 Septemba 1380 katika
familia Albizzeschi kutoka Siena, ambako alihamia baada ya
kubaki yatima, ili alelewe na ndugu zake na
kusomeshwa.
Wito na utume
Akiwa na miaka 22, alijiunga na utawa,
katika tawi la urekebisho wa Waobservanti, ambalo akawa nguzo yake kuu,
pamoja na Yohane wa Kapestrano, Yakobo wa Marka na Alberto wa Sarteano.
Kisha
akaanza utume mkubwa akihubiri kwa mafanikio katika Italia Kaskazini. Kazi
yake yaliamsha katika Kanisa imani na ibada kwa Jina la Yesu na kurekebisha maadili ya wengi. Ndiye aliyesambaza kila
mahali vibao vyenye kifupisho JHS (Jesus
Hominum Salvator) kikiwa na msalaba juu yake na kuzungukwa na jua lenye miali 12.
Kifo
Alifariki
huko L'Aquila, tarehe 20 Mei 1444.
Heshima baada ya kifo
Kutokana na sifa yake kubwa, alitangazwa mtakatifu na Papa Nikolasi V mwaka 1450. Kumbukumbu yake inaadhimishwa kila tarehe 20 Mei.Maisha ya awali
Mwongozo Katika Mkutano wa Sala Kwenye Jumuiya
01.
Maana ya Jumuya Ndogo
Ndogo ya Kikristo (JNNK)
Ni muungano wa familia za kikristo za kikatoliki
kwa ujirani wao kuanzia familia mbili hadi kumi na mbili zinazokutana pamoja
angalau mara moja kwa wiki kwa muda wa saa moja kushirikiana katika kusali,
kusoma Neno la MUNGU na kulitafakari pamoja kujadili na kushirikiana katika
mambo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi kulingana na mazingira yao kwa
madhumuni ya kumtafakari MUNGU na kuuishi ukristo wao kivitendo ili kuwa
watakatifu.
02. Idadi sahihi ya kaya zinazoweza kuunda Jumuiya
Idadi sahihi kabisa, kama vile joto la mwili wa
mwanadamu ni nyuzi joto 37, idadi ya kaya inapaswa kuwa 12. Ishara ya
makabila kumi na mbili ya Taifa la MUNGU na mitume Thenashara. Namba 12
ina utajiri mwingi kimaandiko: Watoto wa Yakobo walikuwa 12 nao ndio waliounda
taifa la MUNGU. Hivyo makabila kumi na mawili, ndio msingi wa jumuiya ya MUNGU.
YESU aliteua Mitume 12, ili waunde taifa jipya la MUNGU. Hivyo nasi
leo, JNNK ni taifa la MUNGU mahalia, idadi ya kaya inayounda zinapaswa kuwa12,
yaweza kukua, ila idadi isipitilize 24, maana yake hapo tutakuwa
tumeshapata taifa/ jumuiya ya pili, yaweza kuwa pungufu, na hapo
itaalikwa kwa namna ya pekee kuinjilisha ili idadi yake ifikie 12. Jumuiya
ikiwa na kaya chache yaani 12 hakutakuwa na kutegeana, wala ubaridi.
03. Faida ya JNNK kwa mkristo mkatoliki
Faida za JNNK kwa mkatoliki ni nyingi, ni vigumu
kuzielezea zote kwani kila mmoja inamgusa kwa namna yake. Zifuatazo ni
fadida chache.
b. Kwa kaya: Kushirikishwa katika masuala ya kiroho. Inasaidia kaya kuishi maadili ya kikiristo hasa, inavyoshirikisha kaya nzima baba, mama, watoto na ndugu wanaoishi nao hivi wanakuwa na nguvu ya kuishi pamoja. Inasaidia ukuzaji wa Imani ya wanakaya.
c. Kwa Kanisa: Inasaidia kuimarisha uhai wa Kanisa. Kwani matendo ya Kanisa yaweza kuonekana Zaidi katika JNNK kuliko katika ngazi za juu za Kanisa. Ni kioo cha uhai wa Kanisa, kwani Kanisa lililo hai ni lile lenye Jumuiya hai. Uinjilishaji wa kina wa Kanisa hufanywa hapa kimatendo.
d. Kwa jamii: Hutoa msaada wa kijamii kwa watu wanaoizunguka bila kujali kama ni wakristo au la. Ni chumvi kwa jamii nzima inayowazunguka. Hata wasio wakristo wanaguswa. Ni mfano halisi wa umoja na ushirikiano kati ya Wakristo na watu wengine.
Mtakatifu Papa Yohane Paulo alisema haya juu ya tabia ya JNNK:
“… kwanza lazima ziwe sehemu za kujishughulisha na
kujitangazia injili yenyewe, ili nao waweze kuwaletea Habari Njema wengine;
Zaidi ya hayo lazima jumuiya ambazo huomba na kusikiliza Neno la MUNGU,
kuhimizana kwa washiriki wenyewe kuchukua wajibu, kujifunza kuishi maisha ya
kikanisa na kutafakari juu ya shida mbalimbali za kibinadamu katika mwanga wa
kiinjili. Zaidi ya yote Jumuiya hizi lazima ziishi maisha ya upendo wa
KRISTO kwa wote, upendo unaopita mipaka ya muungano wa ukoo, makabila au vikundi
vingine.”
Hivyo, mkristo yeyote anayetaka kujua faida ya
Jumuiya shiriki kikamilifu na kwa udumifu maisha yake, utaona uhondo wake kama
vile waswahili wasemavyo kuwa ukitaka kujua uhondo wa ngoma, ingia ucheze.
04. Ukaaji katika Jumuiya wakati wa mkutano wa sala
Mkao wake mzuri na unaohimizwa unapaswa kuwa wa
duara. Wanajumuiya wote waonekane. Hii ni muhimu sana kwani katika
kushirikishana neno kutakuwa hakuna kutegeana, wala ubaridi. Ili kuweza
kufanya duara hili, ni vigumu kama Jumuiya ina kaya zaidi ya 12. Mkao katika
Jumuiya usiwe kama ule ukaaji wa kanisa, la hasha, bali uwe kimduara ili kila
mwanajumuiya aonekane vizuri katika kuleta ushiriki hai. Muda wa sala
katika Jumuiya unatakiwa uchukue saa moja tu na si zaidi ya hapo. Pia,
wanajumuiya wanatakiwa kupanga muda wa kukutana ambao utawawezesha wanajumuiya
wengi kuweza kushiriki bila vipingamizi. Mfano wanaweza kukutana kila
Jumamosi asubuhi kuanzia saa 12:30 hadi saa 1:30 asubuhi.
05. Maji ya Baraka kwenye Jumuiya
Ni vizuri wakati wa kusanyiko la sala kwa
wanajumuiya, kuwepo na Maji ya Baraka yanayowekwa mahali pazuri panapoonekana
vizuri, na wanajumuiya wenyewe wanapofika wanaweza kuchovya vidole katia Maji
ya Baraka na kujibariki, kama ishara ya kukumbuka ubatizo wao, na hivyo kukiri
kwamba sisi sote tuliopo hapa ni ndugu moja, tumejumuishika kutokana na ubatizo
wetu mmoja.
06. Msalaba
Kila Jumuiya inatakiwa kuwa na Msalaba wenye mwili
uliobarikiwa, ili kila wanajumuiya wakutanikapo kwa sala msalaba huo uwepo na
uwekwe katikati ya kusanyiko, yaani katikati ya mduara uliofanyizwa na ukaaji
wa wanajumuiya.
Hebu tutazame kwa ufupi uhusiano wa msalaba na JNNK
Msalaba unajengwa na mbao mbili, moja yatoka kulia
hadi kushoto na ya pili yatoka chini hadi juu. Mbao inayotoka chini hadi
juu ni kiwakilishi cha uhusiano wetu na MUNGU, na ubao utokao kulia hadi
kushoto unawakilisha uhusiano wetu na jamii, na majirani zetu. Mbao mbili
za msalaba zinafanana na Mbao mbili alizopewa Musa (Kut. 32: 15 na kuendelea).
Mbao mbili za Torati, ubao mmoja ulikuwa na amri ya kwanza mpaka ya tatu.
Ni amri zinazoelekeza uhusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake.
Ubao wa pili ulikuwa na amri ya nne hadi yak um, zinazoelezea uhusiano wa
mtu na mtu.
Mkusanyiko wowote wa kijumuiya una mambo haya
mawili, tunakusanyika majirani na mkusanyiko wetu ni wa kumsifu MUNGU. Mkusanyiko wa JNNK ambao MUNGU si kilele chake, mkutano huo hauna tofauti
yoyote na asasi isiyo ya serikali. Na kama mkusanyiko wetu kwa ajili ya
kumsifu MUNGU, bila kumjali jirani, huo ni unafiki mtupu. Kuna hatari ya
JNNK kuwa ni unafiki mtupu au kuwa ni asasi isiyo ya serikali, ndio maana
lazima kila mnapokutana muwe na msalaba katikati yenu uwakumbushe wito wenu.
Tukumbuke: “Mtu akisema anampenda MUNGU, naye anamchukia ndugu
yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi
kumpenda MUNGU ambaye hakumwona” (1 Yoh 4:20).
Msalaba wa KRISTO ni sadaka, na bila sadaka maisha
ya JNNK hayawezekani. Kila mmoja anapaswa kujitoa sadaka kwa ajili ya
mwenzake.
Mfano, Ndugu Muda, yeye hawezi kwenda katika
Jumuiya kwa sababu hana muda. Kazi zake zinambana mno, toka Dominika hadi
Dominika. Lakini mtu huyu huyu ana nafasi ya kutazama tamthilia au mechi
za mpira wa miguu katika luninga, katika vikao vya harusi yeye ndiye wa kwanza
kufika ili kamati zikiundwa achaguliwe katika kamati ya vinywaji na kila siku
hakosekani katika baa. Ukimwambia hili atakujibu kule naenda kupunguza
mawazo kidogo. Lakini muda wa kuondoa uzito wa ubinafsi hana!
Ndugu Muda, kama kweli MUNGU ana nafasi katika
moyo wake, nina uhakika atapata muda wa kushiriki ibada katika JNNK.
Inafaa pia kuwaomba wana jumuiya wenzako kurekebisha mara moja moja
ratiba ili kumuwezesha yeye naye kuwa hai pamoja na wanajumuiya wenzake.
Ndugu Michango, yeye amechoshwa na michango katika
Jumuiya. Alinihesabia, mchango wa maendeleo ya kanisa, mchango wa ujenzi
wa choo, mchango wa shilingi 10,000 kwa kila mbatizwa kwa watu wakubwa na
shilingi 5,000 kwa kila mbatizwa mtoto, mchango kwa ajili ya mwanajumuiya
aliyelazwa na bado kwa kila Dominika kuna sadaka mbili hadi tatu.
Kwa kweli hapa lazima tujiulize swali moja tu, je,
michango hii yote ni kwa ajili ya kuchezea Kamari au kwa ajili ya ulevi?
Je, tukisha ikusanya michango hii tunakwenda kutupa chooni? Kama ni
michango kwa shughuli zenye umuhimu kwa ajili ya kuwapatia jirani zetu ukarimu
wa KRISTO, kuendeleza na kuleta ustawi wa maendeleo ya parokia, hatuwezi
kuepukana nayo. Tunatakiwa kutoa kwa moyo na kwa furaha kulingana na
uwezo wa kila mtu.
Wahenga walituasa, kidole kimoja hakivunji chawa!
Hatuwezi kuushinda uovu katika ubinafsi wetu, kwa kushirikiana pamoja
ndani ya Jumuiya twaweza kabisa kumshinda adui yetu shetani. Hivyo,
tujitahidi sana kadiri tuwezavyo kuvishinda vikwazo vyote vinavyo tuzuia
tusishiriki Jumuiya. KRISTO mwenyewe ametuonesha njia, kwa kutanguliza
kwanza mapenzi ya BABA, na si kutanguliza matumbo yetu au furaha zetu,
malimwengu upitao kama upepo wa kisurisuri.
07. Je, ni masomo gani yanayofaa kusoma kwenye Jumuiya?
Endapo wanajumuiya wameamua kusoma masomo ya Dominika
inayofuata, ni vizuri kama ni lazima kusoma somo la Injili, kwani ndio tui na
kilele cha masomo yote. Ila tu tukumbuke kuwa Maandiko Matakatifu yote
toka kitabu cha Mwanzo hadi cha ufunuo, yafaa kwa kutuongoza katika njia iliyo
nyofu. (2 Tim 3:16).
Pia, wanajumuiya wanaweza kusoma somo linaloendana
na hitaji la Jumuiya. Mfano wanajumuiya wakienda kumtembelea mgonjwa au
wanataka kuombea wagonjwa, wanaweza kusoma somo linaloelezea YESU akiponya
wagonjwa n.k.
08. Ni nani atoe tafakari ya Injili au somo lililosomwa?
Kwanza ni vizuri tufahamu kwamba tunapozungumzia
Jumuiya tunazungumzia ushirikiano, hivyo hata katika ibada zetu twatenda
pamoja. Hivyo si sahihi kusema nani aongoze tafakari. Nimewahi
kukutana na mtu ambaye hakuwa anaenda kusali na wenzake, na tatizo lake ni kuwa
hakuwa na uwezo wa kuongoza tafakari, hivyo aliogopa kwani siku itakapokuwa
zamu yake, angelazimika kuongoza pasipo kutaka. Au unakuta Jumuiya kila
siku ya kukutana ni Mwenyekiti au Katibu wa Jumuiya ndiye anayeongoza tafakari
na kama hayupo siku hiyo tafakari haipo!!
Kila mmoja wetu baada ya kusikia somo mara mbili,
yafuatayo yaweza kumwongoza katika tafakari yake binafsi moyoni, kabla
hajawashirikisha wenzake:
Je, somo
nililolisikia limenigusa nini mimi moyoni mwangu? Kitu ambacho uliposikia tu,
kilifanya nafsi yako, igundue kitu kipya, katika mahusiano yako na MUNGU,
mwenzako wa ndoa, wanakwaya wenzako na jirani kwa ujumla. Ni sawa na mama
yule aliyekuwa anamsikiliza YESU, aliguswa na neno lake ndio maana alipaza
sauti yake na kusema: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha” (Lk
11:27). Mama huyu aliguswa na Neno Lake.
Somo nililolisikia
limenisaidiaje? Mimi kama mimi nimejitambuaje, nina uwezo au mapungufu
gani, sijatimiza wajibu wangu? Je, somo hili limenisutaje nafsini mwangu?
Tusiachie tu kuwa limenigusa, baada ya kunigusa, limekuelekeza katika
changamoto gani ya kuyafanya maisha yako yawe bora Zaidi. Hili ndilo
lililowatokea watu wa Yerusalemu baada ya kusikiliza hotuba ya Petro, waliuliza:
“Ndugu zetu, tufanye nini?” (Mdo 2:37).
Nimebadilishwaje na
somo hili ambalo limenigusa, limenisaidia, na sasa napaswa kutenda jambo Fulani
kama mwitikio wangu kwa hilo neno. Wengi wetu tunapenda kuishia na
kuguswa tu, wachache tu tunaruhusu neno hilo kuwa la msaada katika maisha yetu.
Hatua hii ya tatu ni ya utendaji: “Lakini iweni watendaji wa neno, wala
si kuwa wasikilizaji tu …” (Yak1:22). Zakayo mtoza ushuru anatufundisha
juu ya hatua hii kwa kauli aliyoitoa mbele ya kadamnasi iliyokuwa ikimfuata
YESU: “Sikiliza BWANA! Mimi nitawapa masikini nusu ya mali yangu, na kama
nimemdanganya mtu yeyote kitu, nitamrudishia kiasi hicho mara nne” (soma Lk 19:
1-10).
Hivyo tukisha lisikiliza neno, kila mmoja wetu
ananafasi ya kutushirikisha nini kilichomgusa katika somo hilo, amesaidiwaje na
somo hilo na hasa atuambie atatenda nini kulinga na changamoto aliyoipata
kutokana na somo hilo. Hivyo, tafakari ni tendo ni tendo lenye hatua tatu
katika kutusaidia kuishi ushuhuda wa Habari Njema. Hivyo hakuna
mwanajumuiya ambaye anaweza kudiriki kusema kwamba yeye hawezi kushiriki
tafakari, labla kama ameamua kwa makusudi kufunga masikio ya moyo wake.
Neno la MUNGU lenyewe lina nguvu kutugusa, kutuelekeza, kutupongeza,
kutuonya na kutubadilisha, kama alivyosema Nabii Isaya: “Maana kama vile mvua
ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni wala hairudi huku; bali huinyeshea
ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye
chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa change;
halitarudi bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo
yale niliyolituma” (Isa 55:10-11).
09. Kugawa Jumuiya
Kuwepo kwa kaya nyingi katika JNNK na kisha
wachache wakawa wanashiriki katika Ibada ni dalili ya watu kuona ni vigumu
kuendesha JNNK katika wingi huo.
Kugawa Jumuiya kigezo ni kimoja tu ni eneo
wanaopakana kaya 12 ziunde JNNK moja. Kuna sehemu nyingine tatizo kubwa
kwao la kugawa Jumuiya yenye kaya zaidi ya 24, ni kuangalia nani anapochi
nene, nani anatoa michango mikubwa kunapokuwepo na hitajiko. Kama waamini
watakuwa na mtazamo huu, wajiulize mara mbilimbili, Ukristo wao ni pesa au
Imani yao? YESU alituasa: “… Hamwezi kumtumikia MUNGU pamoja na mali” (Mt
6:24).
Angalisho hapa ni kuwa tendo la kugawa JNNK lisiwe
la pupa tu, badala ya mgawanyo huu kuimarisha ushiriki wa wanajumuiya, ukawa
chanzo cha kufa kwa JNNK. Kwamba hata wale wachache waliokuwa wanasuasua
kufika nao mkawavunja moyo. Hivyo uelimishwaji unapaswa kufanyika, na
sala kumwomba ROHO wa KRISTO, ambaye ni ROHO wa umoja, awaongoze katika nia
yenu njema, inapaswa kusaliwa.
Mara nyingi na sehemu nyingi, waamini wanapenda
kuwa na Mwongozo wa kuendesha Mkutano wa sala kwa kila wanapokutana wenye
kufanana kwa Jumuiya zote. Jambo hili ni la muhimu sana, ila hapa kuna
angalisho la msingi kabisa. Mwongozo huu uwe katika mambo machache ya
msingi, usitake kutoa maelekezo kwa kila kitu. Hili ni la muhimu kwa
sababu JNNK ndio chemchemi ya uhai wa Kanisa. Chemchemi ni eneo tete ambalo
halipaswi kusumbuliwa na mizigo ya sheria, kwani kuna hatari ya kukausha
ubunifu. Ni katika JNNK pekee utamadunisho wa kweli waweza kutokea, na
ili uweze kutokea zinapaswa kuachiwa uhuru katika mambo kadhaa, tena ya msingi
tu. Tuzingatie kwamba: “… na pale palipo na ROHO wa BWANA ndipo ulipo
uhuru” (2 Kor 3:17).
Nitoe mfano mmoja, katika mwongozo wa utaratibu wa
sala, twaweza kusema kila juma kuwepo na ibada ya JNNK, na iwe angalau kwa muda
wa saa moja. Nini cha kufanya katika muda huo wa saa, hapa JNNK inapaswa
kuwa huru kwa chaguo mbalimbali na kwa ubunifu. Mambo ya kuzingatia ni
uwezo wa wanajumuiya, uwingi wao, mahitaji yao kwa siku hiyo ya ibada, ni
kipindi gani cha kalenda ya kiliturujia na eneo wanalokutanika.
Kuna mambo ambayo kwa kila ibada yatakuwepo:
kujuliana hali, kupeana majukumu na sadaka. Lakini kuna mambo
ambayo wanajumuiya wanaweza kuyanyambulisha ambayo watayaingiza katika yale
ambayo ni ya kila siku:
i. Kutafakari Injili, ama kuanza kusoma Injili na kurudia mara mbili baada ya ukimya na kila mtu kusema imemgusa vipi katika maisha yake au kusema tukio lililokugusa katika juma hilo na wanajumuiya kujaribu kuona Maandiko Matakatifu yanatoa mwanga gani wa kuelewa au kuitikia changamoto ya tukio hili.
ii. Kama ni mwezi wa Mbarikiwa Bikira MARIA wanaweza kusali Rozari. Napo kuna njia mbili, kusali Salam MARIA kumi baada ya kila fungu la rozari, ama kusoma sehemu ya Injili inayoelezea fungu husika.
iii. Kama ni wakati wa Kwaresma, wanajumuiya baada yay ale ya kawaida, wanaweka katikati yake sala ya Njia ya Msalaba.
iv. Kama siku hiyo wanamtembelea mgonjwa wanaweza kusali Ibada ya Wanajumuiya kwa Mgonjwa.
v. Kama kuna ubatizo unaotolewa katika Jumuiya wanaweza kuamua kusoma katika Katekesimu ya Kanisa Katoliki, Kanisa linafundisha nini juu ya sakramenti hiyo. Kitabu hiki ni cha muhimu sana katika Imani yetu, ukitoa Biblia Takatifu naweza kudiriki hiki chafuatia kwa umuhimu.
UTARATIBU WA JUMLA
a) Kwa jina la BABA…
b) Wimbo wa Mwanzo
Unaweza kuwa wimbo wa kumwalika ROHO MTAKATIFU au
wimbo wowote unafaa kulingana na kipindi cha Kalenda ya Kiliturujia.
Wanajumuiya wanajuliana hali kama wote ni wazima au kuna mgonjwa kati yao ili waweze kumwombea katika sala na maombi yao n.k.
d) Somo
Somo lililoandaliwa linasomwa kwa mara ya kwanza kwa taratibu, kwa uchaji na kwa sauti inayosikika na wanajumuiya wote
e) Ukimya Mtakatifu
Kisha somo kusomwa kwa mara ya kwanza, unafuata ukimya mtakatifu ili wanajumuiya walitafakari somo kwa kimya ili kuona somo limemgusa kiasi gani na ninatoa changamoto gani katika maisha yake. Ukimya huu waweza kuwa dakika tatu hadi tano.
f) Kurudia kusoma somo lile lile kwa mara ya pili
Somo linarudiwa kusomwa kwa sauti ya kusikika. Si lazima mtu yule yule aliye soma kwa mara ya kwanza kurudia kusoma. Mtu mwingine aweza kusoma.
g) Kushirikisha tafakari
Kila mtu atoe tafakari jinsi ambavyo somo limemgusa katika maisha yake na kusema tukio lililomgusa katika juma na somo limempa changamoto gani katika maisha yake na linamtaka afanye nini.
h) Maazimio
Kutokana na changamoto za somo, au mahitaji ya Jumuiya, wanajumuiya wanaweza kwa pamoja kuweka maazimio ya shughuli au majukumu ya kuyafanyia kazi kwa wiki inayofuata kabla ya mkutano mwingine wa sala.
i) Maombi
Wanajumuiya wanaalikwa kutoa maombi mbalimbali kulingana na mahitaji ya mtu binafsi, familia, Jumuiya, Parokia, kanisa kwa ujumla na marehemu waliotutangulia. Muda wa maombi utazamwe kwani kila mwanajumuiya akitoa ombi lake na kila ombi likichukua muda mrefu, inaweza kuchukua muda mwingi. Maombi yatolewe kwa ufupi na kwa ufasaha.
j) Kukiri Imani
Wanajumuiya wanakiri Imani (Sala ya Nasadiki) v kwa pamoja.
k) Mchango
Baada ya maombi, unafuata mchango (sadaka- kama tulivyozoea kuita).
l) Matangazo
Kisha Mchango, kutolewe matangazo mbalimbali. Matangazo haya pia yanatakiwa kutolewa kwa ufupi ili muda mwingi wa sala usichukuliwe na matangazo
m) Ibada ya kukabidhi Msalaba Mtakatifu familia nyingine
Mwenyekiti / Kiongozi wa Jumuiya:
Tumsifu YESU KRISTO! Ndugu zangu katika KRISTO, napenda kuwajulisha
kuwa leo tutakabidhi Msalaba Mtakatifu kwa familia ya Ndugu…
Somo: Hesabu 21:4-9
Wakasafiri toka mlima Hori kwa njia ya Bahari ya
Shamu, ili kuizunguka nchi ya Edomu: watu wakafa moyo kwa sababu ya ile
njia. Watu wakamnung’unikia MUNGU na Musa, Mbona mmetupandisha huku
kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala
hapana maji na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. BWANA akatuma
nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi
kwa sababu tumemnung’unikia MUNGU, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee
nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. BWANA akamwambia Musa,
Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa,
atazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti,
hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
Neno la BWANA (W). Tumshukuru MUNGU.
Kiongozi wa Jumuiya: Ee MUNGU Mwenyezi na mkarimu,
utuangaze kwa wema, sisi tuliokusanyika hapa, kutambua upendo wako kwetu.
Utujalie moyo wa kudumu katika Imani, Matumaini na Mapendo na kama
ulivyokuwa kule Jangwani yule nyoka wa shaba aliyewekwa juu ya mti, na
walipomtazama, wakaponywa na sumu ya nyoka, tunakuomba sote tutakaomtazama YESU
aliyetundikwa msalabani kwa Imani kuu, tuponywe na sumu yote ya yule mwovu
shetani. Tunakuomba utuimarishe kiimani. Tunaomba hayo kwa njia ya KRISTO
BWANA wetu.
Amina.
Kisha sala hiyo, maandamano ya kusindikiza Msalaba
Mtakatifu yanaanza hadi kwenye kaya ambayo utafanyikia mkutano mwingine kwa wiki
inayofuata, huanza mara moja wanajumuiya wote wakiandamana kwa furaha
wakiongozwa na Msalaba. Wafikapo mahali husika Kiongozi au mwanajumuiya
yeyote aliyeandaliwa atanyunyizia sehemu ya nyumba ya wanafamilia maji ya
Baraka na wanajumuiya wananyunyiziwa maji hayo huku wimbo ufaao ukiimbwa kwa
furaha. Baada ya tendo hilo, wanajumuiya wanatakiana Amani na kumalizia
kwa sala ya “Tunaukimbilia…” Kisha: Mtakatifu … Somo wa Jumuiya yetu
utuombee.
Mwenyekiti / Kiongozi: Nendeni na Amani
Wanajumuiya wote: Tumshukuru MUNGU.
Kisha wanajumuiya wote wanatawanyika kwa furaha
wakimtukuza MUNGU na kwenda kuliishi lile Neno walilolisikia na kutekeleza
wajibu waliopangiana kama upo kwa sifa na utukufu wake MUNGU ili wanadamu
waupate wokovu kwa njia ya KRISTO BWANA wetu.
Subscribe to:
Posts (Atom)
